HALI ya elimu nchini hairidhishi na inatisha. Kutokana na
kutambua umuhimu wake, nimemwandikie barua Mheshimiwa Rais Jakaya
Kikwete, nikitoa mapendekezo ambayo mimi na wanachama wenzangu wa
NCCR-Mageuzi, tumeona yanaweza kuleta tiba kama si kupunguza tatizo.
Mhe. Rais, katika muktadha wa mapendekezo tunayoyaleta kwako tunazingatia masuala ya kitaifa yafuatayo;
(i)
Tangu taifa letu lipate uhuru wake mwaka 1961 (kwa Tanganyika) na mwaka
1964 (Mapinduzi ya Zanzibar) tulitambua umuhimu wa kufuta ujinga, kwa
kuelimisha wananchi ili tujiletee maendeleo. Ingawa hadi sasa kazi kubwa
imefanyika katika kukuza elimu hapa nchini, bado hatujafika katika hali
ya kuwa na taifa ambalo karibu kila raia mwenye umri stahiki anajua
kusoma na kuandika.
(ii) Katika Dira ya Maendeleo ya Taifa ya
2025, tunataja pamoja na mambo mengine kwamba, ifikapo mwaka 2025 tuwe
tumejenga taifa la watu walioelimika kwa upeo wa juu katika nyanja
mbalimbali.
(iii) Tanzania ni miongoni mwa nchi wanachama wa Umoja
wa Mataifa, ambao una malengo nane ya milenia; lengo la pili likiwa ni
upatikanaji wa elimu bora kwa wote.
(iv) Ifikapo mwaka 2015
(takriban miaka miwili toka sasa) tutalazimika kama taifa kupima
utekelezaji wa malengo hayo ili kuendana na viwango vya kimataifa.
Mheshimiwa Rais,
Wakati
tukikabiliwa na malengo hayo ya Kitaifa, kwa muda mrefu kumekuwepo na
viashiria vingi vinavyoonesha kwamba ubora wa elimu itolewayo hapa
nchini katika ngazi zote hauridhishi. Viashiria hivyo ni;
(a) Matokeo
ya hivi karibuni ya mitihani ya kidato cha nne nchini yanaonesha
kuendelea kushuka kwa viwango vya ufaulu wa wanafunzi.
(b) Taarifa
mbalimbali zimeonesha kuwa wanafunzi wengi wanaohitimu elimu ya msingi
na kujiunga na elimu ya sekondari wana uwezo mdogo katika stadi za
kusoma na kuandika na wengine hawawezi kabisa kusoma wala kuandika.
(c)
Shule nyingi za umma zinakuwa na matokeo mabaya ya mitihani
ikilinganishwa na zile zinazomilikiwa na watu binafsi au mashirika
yasiyo ya kiserikali.
(d) Tanzania inashika nafasi ya ngapi kielimu katika Afrika Mashariki?
Athari za udhaifu wa elimu kwa taifa
Mheshimiwa Rais,
Athari za udhaifu katika elimu itolewayo nchini zinajidhihirisha katika sura mbalimbali, miongoni mwazo ni hizi zifuatazo;
i. Kumong’onyoka kwa mila, desturi na utamaduni wa jamii ya Watanzania.
ii. Kuporomoka kwa uadilifu miongoni mwa watumishi wa umma na kada nyinginezo na hivyo ongezeko la ufisadi na rushwa.
iii. Kuporomoka kwa uwajibikaji.
iv. Kuporomoka kwa kiwango cha utii wa sheria na kanuni mbalimbali.
v. Kutothamini rasilimali za taifa.
vi. Tabia ya Watanzania wengi kutothamini matumizi ya muda.
vii. Kupungua kwa uzalendo kwa baadhi ya wananchi.
viii. Kutojiamini kwa Watanzania wanaohitimu elimu katika ngazi mbalimbali.
ix.
Ukosefu wa nidhamu ya matumizi ya tekinolojia ya habari na mawasiliano
(Tehama), mfano matumizi ya simu nururu (mobile phones) na mitandao ya
kijamii wakati wa kazi bila kuzingatia umakini kwenye kazi mtu
anoyafanya.
Mheshimiwa Rais,
Vilevile udhaifu ulioko katika elimu ndiyo hatimaye husababisha matatizo yafuatayo;
i. Kuporomoka kwa viwango vya huduma zitolewazo katika sekta mbalimbali.
ii. Kuporomoka kwa viwango na ubora wa bidhaa, majengo na miundombinu.
iii. Kuporomoka kwa viwango vya uzalishaji wa bidhaa mashambani na viwandani.
iv. Uharibifu na uchafuzi wa mazingira.
v. Udhaifu katika kukabiliana na majanga mbalimbali kama vile mafuriko na tetemeko la ardhi.
vi.
Udhaifu katika kuzuia na kudhibiti ajali zinazoweza kuzuilika, kama
vile ajali za vyombo vya usafiri, moto na milipuko ya silaha.
vii.
Udhaifu katika kukabiliana na hatari za kiafya kwa binadamu na wanyama
zitokanazo na uchimbaji migodini na usafirishaji au uhifadhi wa
kemikali.
viii. Migomo ya watumishi wa umma pamoja na makundi ya
kijamii inayojitokeza katika ngazi mbalimbali, vurugu na migogoro katika
jamii.
Chimbuko la tatizo na hatua tulizojaribu Kuchukua
Mheshimiwa Rais,
Baada
ya tafakuri na utafiti wa muda mrefu sasa, NCCR – Mageuzi tumebaini
kuwa, elimu ya Tanzania imedidimia zaidi kupitia mamlaka zinazoisimamia.
Mifano ya matatizo yanayotokana na mamlaka husika ni kama ifuatavyo;
(a)
Kukosekana kwa mitaala ya elimu nchini, ilhali ipo taasisi husika kwa
ajili ya utengenezaji mitaala. Hili ni tatizo kubwa mno linalowafanya
walimu wafundishe wanafunzi bila kuwa na mwongozo wa pamoja na hivyo
kuifanya elimu itolewayo itegemee ufahamu wa mwalimu mmoja mmoja.
(b)
Ukosefu wa umakini katika kuandaa vitabu vya kiada na ziada kwa ajili
ya matumizi ya shule mbalimbali, ilhali ipo taasisi inayoidhinisha
matumizi ya vitabu mashuleni. Vitabu vilivyoandaliwa na vinavyotumika
kwa sasa vina upungufu mkubwa ya weledi na muongozo.
(c) Mfumo wa
mitihani kukosa mwongozo wa kueleweka, japo nchi inacho chombo maalum
kwa ajili ya mitihani ya kitaifa. Imefikia hatua wanafunzi wanapimwa
uelewa wao kwa maswali ya kuchagua majibu na kubahatisha. Japokuwa mfumo
huo ni mzuri kwa usaili na kurahisisha matokeo kutoka kwa wakati, una
uwezo mdogo wa kupima uelewa wa mwanafunzi.
(d) Wingi wa masomo kwa
wanafunzi wa umri mdogo, wanafunzi wa elimu ya awali wamewekewa kiwango
kikubwa cha mzigo wa masomo bila kujali uwezo wao wa ufahamu na
kuzingatia umri pamoja na kwamba wapo wataalam nchini wa mitaala na
mafunzo.
Kadhalika, darasa la kwanza (elimu ya msingi) wanaanza kwa
kufundishwa masomo manane. Hii inashusha uwezo wa mwanafunzi kutambua
mambo ya msingi na hatimaye anajikuta hatambui chochote.
(e)
Kukosekana kwa waalimu wenye weledi kwenye baadhi ya masomo katika shule
za umma, licha ya kwamba nchi inavyo vyuo mbalimbali vya mafunzo ya
ualimu.
(f) Mazingira duni ya kazi yameshusha kwa kiwango kikubwa ari ya kufanya kazi miongoni mwa walimu.
(g)
Mfumo uliopo umeshindwa kufanya ufuatiliaji na ubaini wa matatizo ya
elimu katika ngazi mbalimbali za elimu kwa nchi nzima, licha ya kwamba
taifa linao wakaguzi wa elimu.
Mheshimiwa Rais,
Tunatambua
tatizo lililopo na tumejaribu kupitia kwa wawakilishi wetu katika Bunge
la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kulishirikisha Bunge katika kutafuta
ufumbuzi wa tatizo hili. Bahati mbaya jitihada zetu kupitia huko
hazikufanikiwa.
Itaendelea toleo lijalo.
NA JAMES MBATIA
Post a Comment