Na Mwandishi WetuMUZIKI
mzuri ulipigwa, watu wazuri wakashangilia burudani kali, wakaikubali
shoo ya Wanaume Family huku wengine wakimkubali Juma Kassim ‘Nature’ na
kundi zima la Wanaume Halisi, ilikuwa ni bonge la historia.

Ulikuwa
ni mpambano wa kukata na shoka, uliopigwa Jumapili iliyopita katika
Ukumbi wa Dar Live, Mbagala Zakhem, jijini Dar ambapo mashabiki
walionesha kuyakubali makundi yote mawili kwa kufanya shoo kali pamoja
na wasanii wengine waliosindikiza.
Asubuhi hadi jioni, watoto
walifurahia michezo mbalimbali iliyopo ndani ya ukumbi huo likiwemo
bembea jipya ambalo lilizinduliwa rasmi katika Sikukuu ya Pasaka.

Giza
lilipoingia watu wazima walianza kupashwa moto na Malkia wa Mipasho
Bongo, Khadija Kopa na bendi nzima ya Tanzania One Theatre ambaye
alishusha sebene baab’kubwa na kuwafanya mashabiki waziimbe nyimbo zake,
mwanzo mwisho.
Kuelekea kwenye mpambano, Mic ilikabidhiwa kwa
Ispector Haroun ‘Babu’ ambaye aliamsha hisia za shoo kwa kugonga nyimbo
zake kali zilizobamba kitambo ikiwemo Asali wa Moyo (remix) ambayo
iliitikiwa kwa shangwe kubwa na mashabiki waliokuwa wakidansi kwenye
eneo la kuchezea.

Mara
baada ya Babu kuamsha mzuka wa burudani, Wanaume Halisi ndiyo walikuwa
wa kwanza kutupa karata yao ya kwanza kwa kuwapandisha baadhi ya wasanii
wake wachanga na kupiga shoo kali iliyopata shangwe la kutosha.
Kama
ilivyokuwa kwa Wanaume Halisi, Wanaume Family nao katika raundi ya
kwanza waliwatanguliza wasanii wake wasio na majina makubwa ambao pia
walishangiliwa kwa sana.
Baada ya raundi hiyo ya kwanza, ulikuwa ni
muda wa mapumziko ambapo legend wa Hip Hop Bongo, Profesa Jay aliutumia
vilivyo kushusha shoo classic ambayo ilinakshiwa na DJ mkongwe Bongo, JD
aliyesimama kwenye moja na mbili huku akiwa miongoni mwa majaji wa
mpambano huo.

Baada
ya mapumziko, raundi ya mashambulizi ndiyo ilifuata ambapo Wanaume
Family walikipandisha kikosi kizima cha maangamizi kilichoongozwa na
Chegge na Temba na umati mzima uliofurika ukimbini ulipagawa na kucheza
nyimbo zao kali kama Kichwa Kinauma, Dar Mpaka Moro na nyinginezo.
Pazia
la burudani lilikamilishwa na Wanaume Halisi ambao walipiga nyimbo zao
kali ikiwemo Ndege Tunduni na umati ulilipuka kwa furaha haswa
wakimshangilia Nature.

Hadi
mwisho wa shoo, makundi yote yalifanya vizuri. Wanaume Halisi
walionekana kupendwa haswa kwa mashabiki wengi kumkubali Nature, lakini
Wanume Family walikubalika zaidi kwa kuangusha shoo kali iliyoteka hisia
za watu wengi jukwaani hivyo mashabiki kuugawanya ushindi kwa makundi
yote mawili kulingana na vigezo vyao.

Historia
inaonesha mara ya mwisho makundi hayo yalipokutana katika Ukumbi wa
Diamond Jubilee mwaka 2008, kulikuwapo na vurugu za hapa na pale lakini
asikwambie mtu, shoo ya Dar Live, mwaka huu ilitawaliwa na amani na
mashabiki waliinjoi shoo kistaarabu mwanzo hadi mwisho. Mpango mzima
ulisimamiwa na udhamini wa Serengeti Premium Legar, Pepsi na Vodacom.
Post a Comment