Kocha
wa Yanga, Ernie Brandts, amesema kwamba endapo timu yake itashinda
mechi yake ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara itakayofanyika Jumatano jijini
Tanga tayari itakuwa imejihakikishia kutwaa ubingwa wa ligi hiyo.
Brandts alisema kuwa baada ya ushindi wao wa juzi wa mabao 3-0
dhidi ya JKT Oljoro kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, haoni
kikwazo cha kutwaa ubingwa ikiwa watapata pointi nyingine tatu ugenini
jijini Tanga.
Mholanzi huyo alisema kuwa kikosi chake kimeimarika zaidi na
kiwango cha juu walichokionyesha katika mechi yao dhidi ya Oljoro
kimempa matumaini makubwa ya kutwaa ubingwa kabla ya mechi yao ya mwisho
watakayovaana na mahasimu wao wa jadi, Simba.
Kocha huyo alisema kuwa anataka kuona Jumatano wanashinda ugenini
na kujiweka katika nafasi nzuri kabla ya kukutana na watani zao wa jadi,
Simba katika mechi itakayofunga msimu wa ligi.
Aliwapongeza pia wachezaji wake kwa kutumia vyema nafasi walizopata
na kuhitimisha mwendo wa kusuasua wa kupachika mabao ulioonekana katika
mechi zao za hivi karibuni, akisema kuwa hayo ni matunda ya kazi kubwa
waliyoifanya kwa wiki mbili kabla ya mechi ya juzi.
''Wiki mbili zote nilikuwa nikiwapa mazoezi ya kufunga, tena kila
mchezaji... mwishowe magoli yamepatikana. Nitaendelea kuwapa mbinu zaidi
wachezaji wangu,'' alisema kocha huyo.
Aliongeza kuwa ushindi wa keshokutwa Jumatano utaondoa hofu dhidi
ya Azam ambao wako katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi.
Alisema kwamba hali za wachezaji wake wawili walioumia juzi, Didier
Kavumbagu na Juma Abdul zitajulikana leo kama watasafiri kesho kuelekea
Tanga kuwakabili wenyeji wao JKT Mgambo.
Yanga ndiyo vinara wa ligi ambao sasa wamefikisha pointi 52, wakati
watani zao Simba wakiwa wameshapoteza nafasi ya kutetea ubingwa huku
Azam ambao walitoka sare ya 2-2 katika mechi yao dhidi ya Simba jana
wakiwafuatia katika nafasi ya pili baada ya kufikisha pointi 47.
CHANZO:
NIPASHE
Post a Comment