MANCHESTER United, Manchester City na Real Madridi zimeingia kwenye vita kubwa ya kumwania kiungo chipukizi wa Malaga, Isco.
Isco, 20, amekuwa na mafanikio makubwa kwenye msimu huu akiwa na Malaga na tayari ametwaa tuzo ya mchezaji bora chipukizi wa mwaka wa La Liga. Kiwango chake kimezivutia klabu nyingi za Ulaya kwa sasa kila moja kuonyesha nia ya kutaka kumsajili.
United na City zote kwa pamoja zimeonyesha nia ya kutaka kumsajili kiungo huyo, lakini Malaga wakati wote wamekuwa wakisita kumwachia nyota huyo.
Malaga wamempa mkataba mpya kiungo huyo hivi karibuni, lakini sasa watakuwa na kazi zaidi kumbakiza baada ya Madrid nao kuonyesha nia ya kumtaka. Jose Mourinho ambaye mstakabali wake bado hajajulikana, ni shabiki mkubwa wa Isco na ameshawaambia viongozi wa Real wafanye jitihada za kumnunua kiungo huyo.
Katika hatua nyingine Manchester United imeingia kwenye vita na Tottenham Spurs za kumwania mshambuliaji chipukizi wa Crystal Palace, Wilfried Zaha.
Chipukizi huyo mwenye miaka 20, ameonyesha nia ya kutaka kucheza Ligi Kuu na timu hiyo ya daraja la kwanza haiwezi tena kumzuia nyota huyo anayechipukia kwenye soka la England.
Japokuwa hakuna maombi rasmi yaliyowekwa mezani, hata hivyo United na Spurs ndizo zinazopewa nafasi ya kumnasa winga huyo aliyeicheza England kwa mara ya kwanza dhidi ya Sweden mwezi Novemba mwaka jana.
Klabu zote mbili zimekubali kumwacha Zaha hapo Selhurst Park kwa mkopo hadi mwisho wa msimu, pia zimekubali kuwapa Palace mchezaji moja au wawili kwa ajili ya kuimarisha kikosi chao.
Post a Comment