MUDA mfupi baada ya mechi ya watani wa
jadi, Simba na Yanga wikiendi iliyopita, Kocha wa Simba, Patrick Liewig
amesema hana uhakika na majaliwa yake lakini ametaja mambo manne
yaliyoifanya timu yake ifungwe mabao 2-0 na Yanga.
Akizungumza katika mahojiano maalum,
Liewig raia wa Ufaransa aliuambia mtandao huu kwamba, kikosi chake
kilicheza vizuri lakini Yanga walitumia vizuri nafasi walizopata.
“Tulicheza vizuri kuanzia mwanzo hadi
mwisho wa mchezo tatizo nafasi tulizopata hatukuzitumia vizuri na
badala yake wenzetu Yanga walicheza vizuri na kutumia nafasi
walizopata,” anasema Liewig.
Kocha huyo hata hivyo alisema anaamini
kikosi chake kinachoundwa na wachezaji wengi vijana na wale waliokuwa
hawapati nafasi kikosi cha kwanza, bado kina nguvu ya kufanya vizuri
msimu ujao wa ligi na hata katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika
Mashariki na Kati ‘Kombe la Kagame’.
Liewig alitaja mambo makubwa manne yaliyoikwaza timu yake na kuruhusu kufungwa mabao 2-0 na Yanga;
SAIKOLOJIA;
“Kabla ya kuingia uwanjani si wachezaji tu hata mashabiki wetu wengi
walijua timu yetu itafungwa, sasa kazi kubwa ilikuwa kuwaweka sawa
wachezaji wetu hasa vijana katika hali ya kuhakikisha tunashinda mechi
hii.
“Wakati sisi tukiwaza hivyo, wenzetu Yanga walikuwa wana
uhakika wa ushindi na mbaya zaidi walikuwa wanawaza kuibuka na ushindi
wa mabao mengi zaidi wakidhani kikosi chetu ni dhaifu,” anasema Liewig.
Liewig anakiri kwamba, pamoja na yote hayo lakini benchi la ufundi la
Simba lilijitahidi kuwaweka sawa kisaikolojia lakini timu zilipoingia
uwanjani ni wazi Yanga ilikuwa vizuri kisaikolojia katika ushindi
kuliko wao.
PENALTI YA MUDDE;
Simba ilipata penalti dakika ya 28 baada ya beki wa Yanga, Nadir
Haroub ‘Cannavaro’ kumuangusha ndani ya eneo la hatari aliyekuwa
mshambuliaji wa Simba, Mrisho Ngassa. Penalti hiyo ilipigwa na Mussa
Mudde raia wa Uganda, lakini alikosa.
“Hadi tunapata penalti, Yanga
walikuwa mbele kwa bao 1-0, hivyo kama tungepata penalti ile matokeo
yangekuwa sawa na kuhamsha morali yetu ya kuhakikisha tunapata matokeo
mazuri.
“Siku zote anayepiga penalti huwapa mashabiki uhakika wa
kupata kwa asilimia kubwa, lakini Mudde amekosa na lile halikuwa lengo
lake japokuwa umakini wa hali ya juu ulitakiwa kuwepo,” anasema Liewig.
KULINDA LANGO;
Liewig anasema kwa muda mwingi viungo na hata washambuliaji wake
walikuwa wakilinda lango badala ya kushambulia kutokana na kasi ya
Yanga hivyo kupoteza lengo la kupata ushindi mapema.
“Kama
tungetangulia kupata bao mambo yangekuwa mazuri lakini muda mwingi
wachezaji wangu walikuwa wakilinda lango kutokana na Yanga walivyokuwa
wanashambulia.
“Mchezo huu wa kulinda ungekuwa mzuri kwetu endapo
tungekuwa tunaongoza angalau kwa bao moja, sasa tulikuwa nyuma kwa bao
moja muda mrefu halafu bado tukawa tunalinda lango, hapo unaona jinsi
gani kwamba hata wachezaji wenyewe walikuwa bado na tatizo la
saikolojia kwa kudhani Yanga inaweza kuwafunga mabao mengi zaidi,”
anasema Liewig.
UBINGWA WA YANGA;
Tofauti na mechi nyingine za watani wa jadi zinavyokuwa, mara nyingi
Simba na Yanga hukutana katika mechi za mwisho tena kwa kuwania pointi
muhimu lakini katika mechi ya wikiendi iliyopita, mambo yalikuwa
tofauti na hata Liewig ameliona hilo.
“Yanga ilikuwa tayari bingwa, sisi tulikuwa na uhakika wa nafasi ya
tatu huku tukiwa hatuwezi kupata nafasi ya pili kwa vyovyote hata kama
tungeshinda. Hii ina maana Yanga, ilicheza kwa kujiamini zaidi huku
ikitaka ushindi tu ili iweze kupewa kombe kwa furaha.
“Sisi
tulitaka kucheza kwa kuweka heshima mbele ya mashabiki wetu huku
tukipingana na makelele ya kufungwa mabao mengi na Yanga. Hili lilikuwa
tatizo dogo japokuwa lilionekana kubwa baadaye,” anasema Liewig.
ANAZUNGUMZIAJE MUSTAKABALI WAKE…………….?
Liewig ambaye alijiunga na Simba Januari mwaka huu, anasema baada ya
kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Yanga huku akiwa na msimamo wa
kuendelea kutowatumia wakongwe, hajui mustakabali wa kazi yake utakuaje.
Kocha huyo muda mfupi baada ya kutua Simba, alihakikisha kikosi
kinakuwa na nidhamu na mchezaji aliyeona anaharibu nidhamu kikosini
alimtimua. Katika ‘timuatimua’ yake, Liewig aliwasimamisha wachezaji
Haruna Moshi ‘Boban’, Amir Maftah, Juma Nyosso, Felix Sunzu, Mwinyi
Kazimoto, Paul Ngalema na Abdallah Juma, lakini baadaye aliwasamehe
Kazimoto na Sunzu.
Uamuzi huu wa Liewig uliigawa Simba kwani si mashabiki tu hata
viongozi wapo waliomuunga mkono na wengine walipinga uamuzi wake huo wa ‘kuwatimua’ kikosini kina Boban.
“Uamuzi huu ulikuwa mzuri kwa manufaa ya Simba na ni mapema kuona uzuri
wa uamuzi wangu lakini baada ya muda mtaelewa kwa nini nilifanya vile.
Bado nina imani na wachezaji vijana ninaowatumia na hata akija kocha
mwingine mambo yatakuwa vizuri kwao,” anasema Liewig.
“Kila msimu
unapoisha, viongozi wa timu huketi pamoja na kufanya tathmini yao sasa
siwezi kukuambia kama majaliwa yangu yatakuaje ndani ya Simba lakini
uongozi wenyewe ndiyo utakaojua nini cha kufanya mimi naheshimu mkataba
wangu hapa,” anamaliza Liewig.
Post a Comment